Ban ataka hatua zaidi kutokomeza usafirishaji haramu wa binadamu

Ban ataka hatua zaidi kutokomeza usafirishaji haramu wa binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa nchi wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kuridhia na kutekeleza kikamilifu mikataba mitatu ya Umoja huo, kama njia moja ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte

Taarifa ya Priscilla

Ni manthari palipofanyika kikao cha ngazi ya juu kuhusu ubia thabiti na uratibu wa kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu na kutokomeza utumwa wa kisasa kupitia maendeleo endelevu, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, ambapo Katibu Mkuu ameutoa wito huo.

Mikataba anayotaka iridhiwe na kutekelezwa kikamilifu katika jitihada hizo ni mkataba dhidi ya uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka, mkataba kuhusu utokomezaji wa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake, na mkataba kuhusu haki za mtoto.

“Tunadhamiria kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu. Hatu za pamoja ni muhimu. Leo, zaidi ya wanawake, watoto na wanaume milioni 60 wanakimbia mizozo, mapigano au wanasaka maisha bora. Lakini wanapofanya safari hizi, wengi wanatumbukia katika kunyanyaswa kwa lazima.”

Ban amesema kila mtu anahitaji kulindwa na kusaidiwa

“Kila mmoja anahitaji haki na fursa. Kuendeleza haki za binadamu ni nguzo ya mkakati wetu. Tushirikiane pia kubadilishana taarifa na kuziba maficho salama ya wahalifu”