Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Feltman ataja sababu za kuendelea kustawi kwa ISIL

Feltman ataja sababu za kuendelea kustawi kwa ISIL

Leo kwenye Baraza la Usalama, mkuu wa idara ya masuala ya kisiasa kwenye Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman amewasilisha ripoti ya kwanza ya Katibu Mkuu kuhusu vitisho vya kundi la kigaidi la ISIL akisema kwamba licha ya jitihada ya kupambana nalo, kundi hilo bado ni tishio kubwa kwa usalama na amani wa kimataifa. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Bwana Feltman amesema ISIL inazidi kupanua operesheni zake kwenye maeneo mengine ya dunia ikiwemo Afrika Magharibi na Kaskazini, huku zaidi ya watu 30,000 wakiwa wamesafiri Syria na Iraq kujiunga na ISIL, mwelekeo huo ukiwa unatia wasiwasi sana.

Amesema ISIL imestawi kutokana na ukosefu wa utulivu na utawala wa kisheria huko Syria na Iraq, huku wakitegemea biashara haram ya mafuta, ushirikiano na vikundi vya uhalifu wa kimataifa na ufadhili kutoka nje.

Hatimaye Bwana Feltman akapendekeza hatua za kutatua mzozo wa Syria kisiasa, kuelimisha vijana kuhusu hatari za itikadi kali, kudhibiti ufadhili wa ugaidi, na pengine:

(Sauti ya Bwana Feltman)

“Kuanzia hatua za kuzuia hadi hatua za usalama na sheria kwa uhalifu, nchi wanachama zinapaswa kuimarisha nyenzo zao za kuvunja uwezo wa ISIL wa kupanga na kutekeleza mashambulizi, ikiwemo kupitia mbinu za uchunguzi maalum na ushirikiano baina ya mashirika.”