Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma dhidi ya watumiaji madawa ya kulevya bado finyu- Ban

Huduma dhidi ya watumiaji madawa ya kulevya bado finyu- Ban

Harakati za kinga na huduma kwa watu walioathiriwa na matumizi ya madawa ya kulevya bado hazitoshelezi, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwenye mkutano wa umoja wa mabunge duniani, IPU uliofanyika leo New York, Marekani.

Mkutano huo wa mwaka umelenga kuangalia tatizo la madawa ya kulevya duniani, hali halisi hivi sasa na hatua za kuchukua kuondokana nalo.

Katika ujumbe wake uliosomwa kwa niaba na Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti uhalifu na madawa ya kulevya, UNODC Yuri Fedeotov, Bwana Ban amesema hali si nzuri kwani ni mtu mmoja tu kati ya Sita wanaotumia madawa ya kulevya ndio anapata huduma ya tiba.

Amesema matokeo yake watu wengi wanaendelea kutaabika na kupoteza maisha ikizingatiwa kuwa mwaka 2013 watu karibu Laki mbili walifariki dunia kutokana na matatizo ya kutumia madawa ya kulevya.

Ban amekaribisha hatua kuelekea mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya mwezi Aprili mwaka huu, akisema zitasaidia uwajibikaji wa pamoja na kusaidia katika kupatia suluhu hali hiyo.

Amekumbusha kuwa kushughulikia tatizo la madawa ya kulevya ni muhimu katika kuhakikisha afya na ujumuishi wa watu wote kwenye utekelezaji wa maendeleo endelevu au ajenda 2030.