Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wamiliki na watendaji wa habari wanakutana Paris kujadili usalama kwa waandishi:UNESCO

Wamiliki na watendaji wa habari wanakutana Paris kujadili usalama kwa waandishi:UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) limeandaa mkutano leo mjini Paris, Ufaransa baina ya wamiliki wa vyombo vya habari na watendaji kutoka kanda zote pamoja na nchi wanachama ili kuchunguza njia thabiti za kuboresha usalama wa waandishi wa habari na kukabiliana na ukwepaji sheria kwa uhalifu dhidi ya wanataaluma ya habari.

Katika mkutano huo waandishi wa habari wasio na mipaka kwa kushirikiana na UNESCO wamezindua muongozo mpya kwa ajili ya waandishi wa habari walio katika mazingira ya hatari. Muongozo huo unasema mashirika ya habari duniani yanasimama kidete kwa ajili ya usalama wa wanataaluma ya habari. Muongozo huo wa kurasa 30 unatoa taarifa na ushauri kwa waandishi ili kuwasaidia kabla, wakati na baada ya majukumu yao katika maeneo ya hatari.

Muongozo huu umekuja wakati ambapo kuna ongezeko kubwa la vitisho dhidi ya waandishi wa habari, huku kukiwa na mauaji ya waandishi zaidi 700 wakiripoti habari katika muongo uliopita pekee. Mwaka 2015 zaidi ya waandishi 105 waliuawa na wengi kupewa vitisho, kutiwa gerezani au kutekwa kwa sababu tuu wanatimiza wajibu wao wa kuipasha habari jamii.