Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM atoa wito raia walindwe wakati wa ghasia Darfur

Mtaalam wa UM atoa wito raia walindwe wakati wa ghasia Darfur

Mtaalum huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Sudan, Aristide Nononsi, ametoa wito ukomeshwe uhasama unaosababisha kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama na kibinadamu eneo la Darfur, nchini Sudan. Taarifa kamili na Joseph Msami

(Taarifa ya Joseph Msami)

Bwana Nononsi ameonya kwamba katika kipindi cha wiki mbili, maelfu ya raia wamelazimika kukimbia makwao katika eneo la Jebel Marra kufuatia ongezeko la ghasia.

Amesisitiza kwamba ghasia sio jawabu katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili Sudan. Ametoa wito kwa serikali ya Sudan kuweka mazingira salama ili kuwezesha  Ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa huko Darfur, Sudan, UNAMID na mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja huo kufikia watu walio na mahitaji wakati wowote, na pia kuwezesha ulinzi wa raia wasiojihami.

Mtaalam huyo amesema kwamba ghasia zinazoendelea zimeripotiwa kusababisha ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa haki za kimataifa za kibindamu, ikiwemo uharibifu wa mali ya raia na kufurushwa kwa raia pamoja na majeraha.

Kwa mantiki hiyo Bw. Nononsi ametoa wito kwa serikali ya Sudan kuwezesha mazungumzo ya pande zote yakiwemo makundi yaliyojihami ili kuleta amani na maridhiano