Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu kuhakikisha ulinzi wa haki za wanawake wakati wa kukabiliana na Zika-Zeid

Ni muhimu kuhakikisha ulinzi wa haki za wanawake wakati wa kukabiliana na Zika-Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, amesema kwamba ni muhimu kutilia maanani haki za binadamu wakati wa kukabiliana na janga la kiafya la virusi vya Zika.

Kupitia taarifa iliyowasilishwa na msemaji wake, Zeid ameongeza kwamba sheria na sera ambazo zinadhibiti upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, ni kinyume na makubaliano ya kimataifa na zinapaswa kufutwa na hatua madhubuti kuchukuliwa ili wanawake wapate taarifa, msaada na huduma wanazohitaji ili kuweza kuamua iwapo wanataka kubeba ujauzito au la, na lini wanapotaka kuubeba.

Cecile Poully ni msemaji wa Ofisi ya Haki za bindamu mjini Geneva

“Hakika, udhibiti wa kuenea kwa virusi vya Zika ni changamoto kubwa kwa serikali za Amerika Kusini. Hata hivyo, ushauri wa baadhi ya serikali kwa wanawake kuchelewesha kushika mimba, unapuuza ukweli wa kwamba wanawake wengi na wasichana hawawezi kudhibiti ni lini wanapata ujauzito, hususan katika mazingira ambako kunashuhudiwa ukatili wa kingono.”

Zeid ameongeza kwamba huduma za kiafya zinapaswa kuwasilishwa kwa njia ambayo inazingatia kwamba mwanamke anafanya maamuzi anayoelewa, haki yake ya faragha, hadhi na utu wake unaheshimiwa, na kwamba huduma zinaendana na mahitaji na maoni yake.