Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa, mafuriko na kipindupindu vyasababisha taabu Malawi

Njaa, mafuriko na kipindupindu vyasababisha taabu Malawi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, limesema kuwa taifa la Malawi linakabiliwa na tatizo la kutokuwa na uhakika wa chakula, ambalo ndilo kubwa zaidi kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.

OCHA imesema takriban watu milioni 2.83 hawana uhakika wa kuwa na chakula, na kwamba milioni 2.4 kati yao watahitaji usaidizi wa WFP wa chakula na fedha hadi mwezi Machi, huku mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yakiwasaidia watu walio na uhakika wa chakula kifedha.

Licha ya usaidizi huo, OCHA imesema kuna pengo katika ufadhili, la dola milioni 20, ili kuwezesha mahitaji ya uhakika wa kuwa na chakula, kulingana na serikali ya Malawi.

Aidha, watu wapatai 22,000 wameathiriwa na vimbunga na mafuriko tangu kuanza msimu wa mvua, wakati Malawi ikiwa bado inajikwamua kutoka kwa athari za mafuriko ya mwaka uliopita, ambayo yalisababisha watu 230,000 kuhama makwao.

Milipuko ya kipindupindu pia inaathiri maeneo yote matatu ya nchi hiyo, na kufikia mwishoni mwa mwezi Januari, visa 421 vilikuwa vimeripotiwa, vikiwemo vifo vinane.