Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa DRC na Congo kurejeshwa makwao kwa tuhuma mpya za ukatili wa kingono CAR

Walinda amani wa DRC na Congo kurejeshwa makwao kwa tuhuma mpya za ukatili wa kingono CAR

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA umebaini watu saba ambao huenda ni wahanga wa ukatili wa kingono nchini humo, huku mkuu wa MINUSCA Parfait Onanga Anyanga akilaani vikali matukio hayo akisema ni aibu kwa Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya MINUSCA imesema kwamba walinda amani kutoka Jamhuri ya Congo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wanashukiwa kufanya vitendo hivyo vilivyotekelezwa kwenye maeneo ya Bambari.

MINUSCA imeeleza kwamba imeshafanya uchunguzi wa awali kuhusu kesi hizo baada ya kupewa ripoti kutoka shirika lisilo la kiserikali la Human Rights Watch, tarehe 21 Januari mwaka huu na kuthibitisha kwamba watu hao wamefanyiwa ukatili wa kingono.

Tayari serikali ya DRC na Jamhuri ya Congo zimearifiwa na Umoja wa Mataifa umeamua kurudisha makwao walinda amani 120 kutoka Jamhuri ya Congo pindi uchunguzi thabiti utakapokamilika na walinda amani hao wakitakiwa kusalia kwenye makazi yao huku kile cha DRC kikitakiwa kuondoka.