Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuongeze kasi kwenye kinga na tiba dhidi ya saratani- Ban

Tuongeze kasi kwenye kinga na tiba dhidi ya saratani- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua zaidi kupunguza machungu yatokanayo na ugonjwa wa saratani.

Katika ujumbe wake wa siku ya saratani duniani hii leo, Ban amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa ni sanjari na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yanayotaka kupunguzwa kwa theluthi moja vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ikiwemo saratani.

Amesema theluthi moja ya visa vya saratani vinaweza kuepukika ilhali vingine vinaweza kutibika iwapo utambuzi utakuwa wa mapema na tiba kupatikana haraka.

Ametaja chanjo dhidi ya virusi vya Human Papiloma vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake akisema ni moja ya mbinu ya kukinga.

Ban amesema hata saratani inapokuwa imefikia hatua ya nne ambayo ni ya mwisho bado mgonjwa anapaswa kupatiwa tiba shufaa ili maumivu yaweze kupungua.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaka siku ya leo itumike kuazimia kutokomeza machungu dhidi ya saratani kwa kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika harakati za kinga na tiba