Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya waalbino yanapaswa kukabiliwa kwa pamoja: UN

Mashambulizi dhidi ya waalbino yanapaswa kukabiliwa kwa pamoja: UN

Kamati ya Haki za Watoto ya Umoja wa Mataifa iliyokutana wiki hii mjini Geneva, Uswisi, imewasilisha leo ripoti yake kuhusu baadhi ya nchi zilizoangaziwa mwezi uliopita zikiwemo Senegal, Zambia, Zimbabwe, Benin na Kenya. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Akiwasilisha ripoti yake mbele ya waandishi wa habari, mmoja wa wataalam Jorge Cardona amemulika mateso yanayotekelezwa dhidi ya watoto kwenye nchi hizo akitaja maumivu kwa watoto wanaodaiwa kuwa wachawi, ukeketaji, na mashambulizi dhidi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi, albinism.

Bwana Cardona ameeleza kwamba nchi 16 barani Afrika zinashuhudia mashambulizi ya aina hiyo.

(Sauti ya Bwana Cardona)

“ Mara nyingi yanahusiana na uchaguzi wa kisiasa na yadaiwa viungo vya mwili wao vinaleta baraka. Matukio ya chaguzi za serikali za mitaa au kitaifa nchi jirani yamesababisha ongezeko la mashambulizi na mauaji nchi nyingine jirani. Hivyo tatizo hilo haliwezi kukabiliwa na nchi moja pekee, linahitaji uratibu wa pamoja."