Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zaidi zahitaji kufadhili msaada wa kibinadamu: Eliasson

Juhudi zaidi zahitaji kufadhili msaada wa kibinadamu: Eliasson

Leo Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson amesema hatua za kihistoria zinapaswa kuchukuliwa ili kusaidia watu milioni 125 wanaohitaji usaidizi wa kibinadamu duniani kote.

Amesema hayo akizindua kikao kilichofanyika mjini New York Marekani kujadili ripoti ya wataalam kuhusu ufadhili wa usaidizi wa kibinadamu, akisema

(Sauti ya Bwana Eliasson)

“Licha ya majanga ya asili, dunia inakabiliana na majanga yaliyosababishwa na binadamu. Mateso ni mengi sana na sheria ya kimataifa ya kibindamu inadharaulika kwa kiasi cha kushtua. Vitendo hivyo na hali hiyo ni ukiukwaji wa ubinadamu wetu na maadili ya msingi ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu,”

Bwana Eliasson amesisitiza umuhimu kwa nchi wanachama kushiriki mkutano wa ufadhili kwa mzozo wa Syria unaoanza Alhamis mjini London, Unigereza kadhalika, kongamano la kimataifa la masuala ya kibinadamu litakalofanyika Istanbul, Uturuki mwezi Mei.

Ripoti kuhusu ufadhili wa kibinadamu iliyozinduliwa Januari mwaka huu imeandaliwa na jopo la wataalam lililoongozwa na Sultan Nazrin Shah wa Malaysia na Naibu Rais wa Muungano wa Ulaya Kristalina Georgieva, imebaini kuwa kuna pengo la dola bilioni 15 kila mwaka katika usaidizi wa kibinadamu.

Ripoti hiyo imetoa mapendekezo matatu makubwa: kupunguza mahitaji kupitia harakati za kuzuia mizozo kuibuka tena, kujenga uwezo wa jamii kupunguza athari za majanga. Pili ni kuongeza ufadhili kupitia vyanzo mbadala na bunifu, na hatimaye kuimarisha ufanisi ma usaidizi wa kibinadamu.