Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa kimataifa wa wahisani kwa ajili ya Syria kuanza London:FAO

Mkutano wa kimataifa wa wahisani kwa ajili ya Syria kuanza London:FAO

Viongozi kutoka kila pembe ya dunia wawanakutana London kuanzia kesho Alhamisi kwa ajili ya mkutano wa wahisani wa Syria. Grace Kaneiya  na taarifa kamili

(TAARIFA YA GRACE)

Lengo la mkutano ni kuchangisha fedha ili kukidhi mahitaji ya mamilioni ya watu walioathirika na mgogoro nchini Syria.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO usalama mdogo wa chakula nchini Syria unahitaji kupewa kipaumbele  kwani mamilioni ya watu wanakabiliwa na baa la njaa.

Vita vya Syria vikikaribia miaka sita sasa FAO inasema mfumo uzalishaji wa kilimo umeathirika vibaya .Dominique Burgeon ni mkurugenzi wa FAO wa kitengo cha dharura anafafanua kuhusu hali halisi nchini humo.

(SAUTI YA DOMINIQUE BURGEON)

"Kuna athari za moja kwa moja za kuharibika kwa  miundombinu ya kilimo kama vile mifumo ya umwagiliaji maji, uhifadhi na vifaa vya kilimo. Pia kuna athari zisizo za moja kwa moja ikiwemo kusua sua kwa soko ambako kwa wakulima walio vijijini ni vigumu kwao kupata pembejeo. Hii ina maanisha kwamba uzalishaji unapungua na hivyo kusababisha mamilioni ya watu kukabiliwa na  uhaba wa chakula."