Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia imejitahidi kupambana na ukame, isaidiwe- Ban

Ethiopia imejitahidi kupambana na ukame, isaidiwe- Ban

Baada ya kuhudhuria mkutano wa 26 wa viongozi wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametembelea eneo la Oromia ili kushuhudia ukame mkali zaidi kwa kipindi cha miaka 30 unaokumba nchi hiyo na harakati zinazochukuliwa na serikali.

Kabla ya kutembelea alizungumza na wahisani kwenye kikao maalum kilichofanyika Addis Ababa kuhusu mzozo wa kibinadamu Ethiopia, ambapo alisema janga hilo limezidi uwezo wa serikali ya Ethiopia wa kukabiliana nao, licha ya jitihada kubwa ilizoonyesha, huku akieleza kwamba tayari serikali ya Ethiopia imechangia dola milioni 381 ili kupambana na ukame huo.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu akazisihi nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuongeza ufadhili ili kusaidia juhudi za serikali ya Ethiopia, akiwasihi pia kushiriki Kongamano la Kimataifa la Misaada ya Kibinadamu litakalofanyika mjini Istanbul Uturuki mwezi Mei mwaka huu. Ban alikariri kauli hiyo alipotembelea eneo la Oromio na viongozi wa Ethiopia ambapo Priscilla Lecomte anatupatia taswira halisi kupitia makala hii.