Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi ya Bemba kuamuliwa mwezi Machi ICC

Kesi ya Bemba kuamuliwa mwezi Machi ICC

Uamuzi kuhusu kesi ya Jean-Pierre Bemba, aliyekuwa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC utatangazwa tarehe 21 mwezi Machi mwaka huu na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC.

Taarifa ya ICC iliyotolewa leo imeeleza kwamba Jean-Pierre Bemba ameshukiwa na uhalifu wa kibinadamu na uhalifu wa kivita vikiwa ni vitendo vya mauaji, ubakaji na uporaji ambavyo vinadaiwa kutekelezwa mwaka 2002 na 2003 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Taarifa ya Radio Okapi kutoka DRC imeeleza zaidi kwamba uhalifu huo umetekelezwa na kundi la waasi lililokuwa chini ya uongozi wa Bwana Bemba, MLC, ambalo lilitumwa CAR ili kusaidia rais wake Ange Félix Patassé kupambana na vikundi vilivyojihami.

Bwana Bemba amefungwa The Hague tangu mwaka 2008 kwa madai ya uhalifu huo. Kesi yake imeanza kusikilizwa mwaka 2010 na ikaisha Novemba 2014.

ICC imesema kwamba pande za kesi hiyo zitakuwa na haki ya kutia rufaa.