Skip to main content

Israel yamulikwa kuhusu vizuizi vya kiutawala

Israel yamulikwa kuhusu vizuizi vya kiutawala

Mratibu wa usaidizi wa kibinadamu na misaada ya maendeleo, Robert Piper, ameeleza kusikitishwa na vitendo vya Israel kuendelea kuwa na vizuizi vya kiutawala, na hasa kusikitishwa na hali ya afya ya mahabusu wa Kipalestina, Mohammed Al-Qiq, ambayo inayozorota kasi. Bwana Al-Qiq amekuwa kwenye mgomo wa kususia chakula akiteta dhidi ya kuzuiliwa kwake holela na kuteswa.

Kulingana na takwimu za idara ya magereza ya Israel, Wapalestina 527, akiwemo mwanamke  mmoja na watoto watano, walikuwa wakishikiliwa katika magereza ya Israel hadi mwishoni mwa Novemba 2015.

Bwana Piper amesema, baada ya siku 69 za kususia mlo, Bwana Al-Qiq yumo katika hali tete kiafya, na madaktari wake wamemwambia kuwa huenda kuna madhara yasiyoweza kurekebishwa. Amekariri msimamo wa Umoja wa Mataifa kuwa wafungwa wote wa kiutawala, wawe Waisraeli au Wapalestina, wanapaswa kufunguliwa mashtaka au waachiwe huru mara moja, na madai ya utesaji kuchunguzwa haraka.