Skip to main content

Zaidi ya watu bilioni 1 hutegemea ardhi oevu kuishi, ingawa inapotea- UNEP

Zaidi ya watu bilioni 1 hutegemea ardhi oevu kuishi, ingawa inapotea- UNEP

Ikiwa leo ni Siku ya Ardhi Oevu Duniani, Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP, limesema kuwa zaidi ya asilimia 64 ya ardhi oevu imepotea tangu mwaka 1900, kwa kiasi kikubwa ikigeuzwa kuwa maeneo ya kilimo au kuendeleza makazi ya mijini, na hivyo kuhatarisha maisha ya watu zaidi ya bilioni moja, ambao hutegemea ardhi oevu kuishi.

Ardhi oevu hutegemewa kwa shughuli za uvuvi, kupanda mpunga na kazi za sanaa ya mikono, huku sekta zingine kama vile utalii, usafiri wa majini na ufugaji wa samaki zikitegemea ardhi oevu.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Ardhi oevu kwa mustakhbali wetu: tegemeo endelevu,” leo Februari Pili ikiwa ni miaka 45 tangu kusainiwa kwa agano la Ramsar kuhusu ardhi oevu.

Hafla zaidi ya 800 zimepangwa kufanyika kote duniani kumulika mchango mkubwa wa ardhi oevu kwa maisha bora kwa wanadamu, na kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi hiyo.