Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mashambulizi ya bomu Damascus, ataka mashauriano mema Geneva

Ban alaani mashambulizi ya bomu Damascus, ataka mashauriano mema Geneva

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani mashambulizi matatu yaliyofanywa karibu na kaburi la Sayidda Zeinab kusini mwa Damascus, Syria, hapo jana Januari 31.

Ripoti kutoka kwa serikali ya Syria na wafuatiliaji mashinani zinasema kuwa zaidi ya watu 60 huenda waliuawa, huku zaidi ya mia wengine kujeruhiwa katika shambulizi hilo lililodaiwa kutekelezwa na Daesh/ISIL.

Katibu Mkuu ametuma rambi rambi zake kwa familia za wahanga, na kuwatakia majeruhi uponaji wa haraka, huku akisema wanaotekeleza mashambulizi kama hayo dhidi ya raia ni lazima wawajibishwe kisheria.

Mashambulizi ya jana yamefanyika wakati mazungumzo yakianza mjini Geneva, Uswisi, yakilenga kuutafutia mwarobaini mzozo wa Syria. Kwa mantiki hiyo, Ban amesema watu wa Syria wanatarajia kuona mashauriano ya kuaminika.