Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aelezea wasiwasi kuhusu hali Burundi

Zeid aelezea wasiwasi kuhusu hali Burundi

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al-Hussein, ameeleza wasiwasi wake kuhusu matukio nchini Burundi yanayoonyesha hali kuendelea kuwa mbaya hata zaidi. Taarifa kamili na Assumpta Massoi

(Taarifa ya Assumpta)

Kamishna Zeid amesema hayo akikutana na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, ambapo amesema kuwa atafanya leo mkutano na Mjumbe maalum wa Rais Nkurunziza ili kujadili hali iliyoko nchini Burundi.

Akielezea hofu yake kuhusu mwelekeo wa mzozo wa Burundi, Kamishna Zeid amesema kwamba ofisi yake imekuwa ikifanya jitihada za pamoja na mamlaka za Burundi ili kuona kuwa hali haizoroti zaidi.

Tumefurahi kuwa wanahabari wawili wa kigeni waliachiwa huru Ijumaa iliyopita. Tunazihimiza mamlaka za Burundi ziwaachie huru wafungwa wengine, katika muktadha wa mzozo uliopo sasa. Mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari vilivyofungwa, vinapaswa kufunguliwa pia, kama sehemu ya kujenga imani kwa ajili ya mazungumzo fanisi.”

Kamishna Zeid amesema kuwa madai ya hivi karibuni kuhusu kuwepo makaburi ya halaiki yanaonyesha siyo tu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika, lakini pia unaoweza kufanyika iwapo hali ya sasa haitashughulikiwa.