Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Filamu zimesalia ushawishi kwa watoto kuvuta sigara - WHO

Filamu zimesalia ushawishi kwa watoto kuvuta sigara - WHO

Shirika la afya duniani, WHO limetoa wito kwa serikali kuweka udhibiti kwenye filamu zenye matukio ya uvutaji sigara ili kuepusha watoto na vijana barubaru kushawishika kuvuta sigara na bidhaa za tumbaku.

Wito huo umo kwenye ripoti Filamu bila uvutaji sigara kutoka ushuhuda hadi hatua iliyotolewa leo, ikiwa ni toleo la tatu tangu uzinduzi wa kampeni hiyo mwaka 2009.

Ripoti inasema filamu za aina hiyo zimechochea mamilioni ya vijana ulimwenguni kote kuanza kuvuta sigara na kutokana na udhibiti wa matangazo ya bidhaa za tumbaku, filamu zimesalia mbinu ya kuwashawishi.

Dkt. Douglas Bettcher kutoka idara ya kinga ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza WHO amesema hatua ya udhibiti kwa watoto wasitazame filamu hizo sambamba na maonyo kabla ya filamu kuanza zitaepusha dhdi ya kuanza matumizi, kukumbwa na uraibu na hatimaye magonjwa na vifo.