Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uturuki lazima iheshimu haki za raia-Zeid

Uturuki lazima iheshimu haki za raia-Zeid

Kamishina mkuu wa ofisi ya Umoja wa mataifa ya haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein Jumatatu ameutaka uongozi wa Uturuki kuheshimu haki za msingi za raia katika operesheni zake za usalama na kuchunguza haraka madai ya kuwafyatulia risasi kundi la watu wasiokuwa na silaha kwenye mji wa Kusini Mashariki wa Cizre, baada ya video ya tukio hilo kuonekana juma lililopita.

Zeid pia ameelezea hofu yake kufuatia ripoti kwamba mpiga picha ambaye pia alijeruhiwa atakamatwa pindi akitoka hospitali, na pia hukumu kali ya kifungo dhidi ya waandishi wengine wawili maarufu nchini Uturuki, mhariri mkuu wa gazeti la Cumhuriyet, Can Dündar, na mkuu wa ofisi yao ya Ankara, Erdem Gül.

Video iliyorekodiwa na Refik Tekin ni ya kushtua sana amesema Zeid na hivi sasa Refik Tekin anayeripotiwa kulazwa katika hospitali ya Mardin anasubiriwa na polisi kwenye mlango wa chumba chake akiwa na vibali vya kumkamatwa vilivyosainiwa na gavana na mwendesha mashtaka vikimshutumu Bw Tekin kuwa ni mwanachama kundi lililojitenga la kigaidi.

Kamishna ameongeza kuwa kurekodi video ya vitendo vya ukatili sio jinai lakini kuwafyatulia risasi raia wasiojihami hilo ni kosa.