Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Afrika waongee na sauti moja kuhusu mabadiliko ya Umoja wa Mataifa: Ban

Viongozi wa Afrika waongee na sauti moja kuhusu mabadiliko ya Umoja wa Mataifa: Ban

Mkutano wa 26 wa Muungano wa Afrika ukiendelea mjini Addis Ababa Ethiopia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza kwamba uwakilishi katika Baraza la Usalama ni moja ya kipaumbele cha Umoja wa Mataifa, lakini ni wajibu wa nchi wanachama kuelewana kuhusu mabadiliko wanayotaka kutekeleza.

Bwana Ban amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Addis Ababa, ambapo aliulizwa kuhusu jinsi ya kuimarisha uwakilishi wa Afrika katika mfumo wa Umoja wa Mataifa na hasa Baraza la Usalama, ambalo ni suala lililoibuka katika mkutano wa Muungano wa Afrika.

Katibu Mkuu amesema kwamba karibu  nchi zote wanachama zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kuleta mabadiliko katika muundo wa Umoja wa Mataifa, lakini kila nchi inapigia chepuo maslahi yake. Amewaomba viongozi wa Afrika kuelewana kuhusu mahitaji yao ya pamoja na kuongea kwa sauti moja.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa Muungano wa Afrika kutopeleka vikosi vya walinda amani nchini Burundi, Bwana Ban amesema kwamba kwamba viongozi wa Burundi na raia wake pekee  wataweza kutatua mzozo huo kupitia mazungumzo jumuishi, akiongeza: 

(Sauti ya Ban)

¨Nataka kuunga mkono aina zote za suluhu zitakazoweza kusaidia kukuza amani na utulivu, na kulinda haki za binadamu nchini Burundi. Lakini cha msingi ni jukumu la Muungano wa Afrika, kwa kushirikiana na serikali ya Burundi kuamua aina ya harakati zinazopaswa kuchukuliwa.¨  

Halikadhalika Katibu Mkuu amepongeza Tanzania, Nigeria, Burkina Faso, Côte d'Ivoire na Jamhuri ya Afrika ya kati kwa kutekeleza uchaguzi kwa amani na demokrasia mwaka uliopita.

Kabla ya kuhitimisha ziara yake nchini Ethiopia, Katibu Mkuu alikuwa anatarajiwa kutembelea eneo la Oromo lililokumbwa na ukame mkali uliosababishwa na El-Niño.