Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ki-moon azungumzia mzozo wa Burundi na viongozi wa Rwanda na Burundi

Ban ki-moon azungumzia mzozo wa Burundi na viongozi wa Rwanda na Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemwambia Naibu Rais wa Burundi Joseph Butore kwamba mchakato wa kisiasa unapaswa kuwa jumuishi, endelevu, na kuungwa mkono na jumuiya ya kikanda na kimataifa ili kupata suluhu kwa mzozo unaoendelea nchini humo.

Bwana Ban amesema hayo akizungumza na Bwana Butore leo kuhusu hali ya kiusalama, haki za binadamu na kibinadamu nchini Burundi, kando ya mkutano wa Muungano wa Afrika ulioanza leo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Bwana Ban ameisihi serikali ya Burundi kuendelea kuwa na uwazi kuhusu hali iliyo nchini humo.

Wakati huo huo Bwana Ban amekutana pia na Rais wa Rwanda Paul Kagame, akimelezea wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa hali ya Burundi. Wamezungumzia matokeo ya kibinadamu na kiusalama ya mzozo huo.

Aidha Katibu Mkuu ameipongeza Rwanda kwa jitihada zake katika kuendeleza ajenda ya tabianchi na malengo ya maendeleo endelevu.