Skip to main content

Ban Ki-moon apongeza viongozi wa Afrika wanaoacha madaraka kwa kuheshimu katiba

Ban Ki-moon apongeza viongozi wa Afrika wanaoacha madaraka kwa kuheshimu katiba

Akizungumza leo kwenye ufunguzi wa kikao cha 26 cha Muungano wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewaomba viongozi wa Afrika wafuate mfano wa viongozi wanaocha madaraka kwa kuheshimu katiba za nchi zao.

Ameongeza kwamba uchaguzi ni mtihani kwa utawala bora, huku nchi 17 za Afrika zikitarajia kufanya uchaguzi mwaka huu.

(Sauti ya bwana Ban)

¨Viongozi hawapaswi kubadilisha katiba kwa njia zisizoheshimu demokrasia, wala kutumia mianya ya sheria ili kubaki madarakani. Tumeshaona majanga yanayotokea wakifanya hivyo. Viongozi wanapaswa kulinda wananchi, siyo wao wenyewe. Napongeza viongozi walioacha madaraka na kuheshimu idadi ya muhula iliyodhibitiwa kikatiba.¨

Aidha amewaomba nchi wanachama wanaochangia operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa kuhakikisha walinda amani wanaheshimu haki za binadamu, akiongeza kwamba ripoti za unyanyasaji wa kingono uliofanyiwa na walinda amani zimekuwa aibu kubwa.

Halikadhalika Bwana Ban ambaye anashiriki mkutano kwa mara ya mwisho kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepongeza jitihada za viongozi wa Afrika katika kukuza haki za binadamu na hasa za wanawake, kutokomeza janga la Ebola na kuendeleza mchakato wa amani Sudan Kusini na Burundi.