Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

De Mistura aelezea matumaini ya kukutana na upinzani wa Syria Jumapili

De Mistura aelezea matumaini ya kukutana na upinzani wa Syria Jumapili

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Stafan de Mistura, amesema leo anaamini kuwa ataweza kukutana na kamati kuu ya mashauriano ya upinzani nchini Syria mnamo Jumapili jijini Geneva, Uswisi.

Bwana de Mistura amesema hayo baada ya kukutana na Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Jaafari na ujumbe wa serikali ya Syria.

“Nina sababu nzuri za kuamini kuwa wanalifikiria hili kwa umakini. Na kwa hiyo, ili kuweza kuwa katika nafasi - labda Jumapili - ya kuanza mashauriano ili kuendelea na kuanza mazungumzo baina ya pande kinzani za Syria. Njia bora ya kujadili utekelezaji wa viashiria muhimu kwa watu wa Syria ni kuja Geneva.

Mazungumzo hayo ndiyo ya kwanza tangu awamu mbili za mazungumzo zilipofeli mwaka 2014.

Kufikia sasa, mzozo wa Syria umewaua watu 250,000, kuwalazimu mamilioni ya wengine kuhama makwao, na mamia ya maelfu yaw engine kukimbilia Ulaya.

Bwana de Mistura amesema, la kipaumbele sasa ni usitishaji mapigano, kuwezesha ufikishaji misaada ya kibinadamu, na kukomesha tishio la kundi la kigaidi la ISIS.

Suala bila shaka ni kwamba, aina yoyote ya mazungumzo ya usitishaji mapigano ni kitu tunacholenga, mbali na mazungumzo ya msingi kuhusu mustakhbali wa Syria, yanahitaji kuhusisha pande mbili. Usitishaji mapigano hufanyika kati ya pande zinazopigana. Ndiyo maana kwetu sisi, ni muhimu kuwa na dalili yoyote kuhusu tulipo kuhusu uwepo wa kamati kuu ya mashauriano.”

Akijibu maswali kutoka kwa waandishi habari, Bwana de Mistura amesema kuwa uwezeshaji wahudumu wa kibinadamu kuwafikia wahitaji katika maeneo yaliyozingirwa unapaswa kutekelezwa.

Kuna maeneo 14, baadhi yayo yakiwa yamezingirwa na serikali, mengine na upinzani, na moja na ISIS. Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi watu wa Syria wanavyoteseka kutoka upande mmoja hadi mwingine, na mazungumzo haya yanapaswa kushughulikia suala hilo.”

Bwana de Mistura amesema kuna haja ya kufanya mazungumzo hayo, ili kuweza kushughulikia siyo tu suala la mustakhbali wa Syria, lakini pia kuboresha hali ya watu wa Syria kwa kupunguza ukatili, mashambulizi ya mabomu na kusitisha mapigano.