Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa UM waitaka Marekani kushughulikia ukatili wa polisi na dhuluma za ubaguzi wa rangi

Wataalamu wa UM waitaka Marekani kushughulikia ukatili wa polisi na dhuluma za ubaguzi wa rangi

Alama za utumwa zinasalia kuwa changamoto kubwa nchini Marekani kwa kuwa kumekuwa hakuna ahadi ya kweli kutambua na kuwalipa fidia watu wenye asili ya Afrika, limesema leo jopo la wataalamu wa Umoja mwishoni mwa ziara yao ya pili rasmi nchini humo.

Kuanzia tarehe 9 hadi 29 mwezi huu jopo la wataalamu hao kuhusu watu wenye asili ya Afrika limezuru Washington D.C, Baltimore, Jackson- Mississippi, Chicago, na New York City ili kushughulikia masuala ya sasa, na kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, ubaguzi dhidi ya Uafrika, chuki dhidi ya wageni na kulinda na kukuza haki za binadamu za Wamarekani weusi.

Licha ya mabadiliko makubwa tangu kumaliza utekelezaji wa Jim Crow, kupambana kwa ajili ya haki za kiraia, itikadi za kuhakikisha utawala wa kundi moja kuwa juu ya jingine bado zinaendelea kuathiri vibaya haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kimazingira za Wamarekani weusi hivi leo, amesema mtaalam wa haki Mireille Fanon Mendes France, ambaye kwa sasa anaongoza jopo la wataalamu hao.

Jopo hilo ambalo limejumuisha pia Sabelo Gumedze na Ricardo A. Sunga III, limekaribisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Marekani kushughulikia masuala kama kupiga marufuku kifungo cha upweke kwa vijana wadogo  katika mfumo wa shirikisho la magereza uliotangazwa juma hili.