Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ki-moon aziomba nchi za Muungano wa Afrika kutumia uongozi wao kuleta amani Burundi

Ban ki-moon aziomba nchi za Muungano wa Afrika kutumia uongozi wao kuleta amani Burundi

Burundi, Sudan Kusini na Ugaidi ni mada zilizozungumzwa na Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika lililokutana hii leo Addis Abeba, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewapongeza wanachama wa Muungano wa Afrika na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa jitihada zao katika kuzuia ghasia zaidi nchini Burundi.

Bwana Ban amesema azimio la kuunda Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Burundi MAPROBU limetuma ujumbe mkubwa kwa bara lote na dunia kwa ujumla kwamba nchi za Afrika hazitanyamaza na kushuhudia ukiukaji wa haki za binadamu na ghasia.

Aidha amesihi wanachama hao kutumia uongozi wao wote ili kuanzisha mchakato jumuishi wa amani na kuzuia Burundi kuangukia katika ghasia zaidi.

Kuhusu Sudan Kusini ameuomba Muungano wa Afrika na IGAD wahakikishe kwamba pande zote za viongozi wa Sudan Kusini wanawajibika kutimiza ahadi zao na kuunda serikali jumuishi ya mpito, ili kusitisha mateso kwa raia.

Na kuhusu ugaidi unaolikumba bara hilo, ameziomba nchi wanachama kuunga mkono mpango wake wa kupambana na itikadi kali na ukatili aliuwasilisha hivi karibuni.