Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nishati mbadala nchini Uganda

Nishati mbadala nchini Uganda

Upatikanaji wa nishati kwa wote ni changamoto kwa karne ya 21, wakati ambapo mtu mmoja kati ya watano hawapati huduma za umeme duniani, na Umoja wa Mataifa ukitarajia kuwa mahitaji ya nishati yataongezeka kwa asilimia 33 ifikapo mwaka 2035.

Miongoni mwa malengo ya maendeleo endelevu au SDGs yaliyopitishwa mwaka 2015, lengo namba 7 ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati endelevu kwa wote na kwa bei nafuu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nishati zitokanazo na mafuta au kuni ni hatari kubwa kwa mazingira, na wala hazitaweza kutimiza mahitaji ya watu wote duniani katika miaka ijayo. Uwekezaji katika vyanzo mbadala na jadidifu vya nishati kama vile miyonzi ya jua, nguvu za maji, upepo, ardhi unapigiwa chepuo hivi sasa kama fursa kwa kutunza mazingira na kukuza maendeleo endelevu.

Barani Afrika kwa mfano, Kenya inategemea kuzalisha asilimia 27 ya nishati zinazohitajika nchini humo kupitia jotoardhi au geothermal ifikapo mwaka 2031.

Nchini Uganda, bado asilimia kubwa ya familia hutumia makaa ya mawe au kuni katika shughuli za kila siku. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, hali hiyo inahatarisha uwepo wa misitu nchini humo. Kupitia ushirikiano na serikali , UNDP na mashirika mengine yanajaribu kuwezesha wafanyabiashara kutengeneza makaa ya mawe kwa kutumia vyanzo vingine vya biomasi visivyokuwa miti.

Mwandishi wetu John Kibego ametembelea kiwanda kinachozalisha aina hiyo ya nishati mbadala wilayani Hoima

(Kibego package)