Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mawaziri wakutana kutathmini mkakati wa amani na usalama wa DRC

Mawaziri wakutana kutathmini mkakati wa amani na usalama wa DRC

Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Wawakilishi wa nchi wanachama wa mkakati wa amani, usalama na ushirikiano kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC na ukanda wa Maziwa Makuu (PSC), umependekeza kuwa mikutano ya siku za usoni ya mfumo wa kikanda wa kufuatilia utekelezaji wa mkakati huo, itenganishwe na mikutano mikuu ya Muungano wa Afrika, AU na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ili kuhakikisha kuwa wakuu wa nchi wanachama wanajikita tu katika mazungumzo yanayohusiana na utekelezaji wa mkakati huo.

Pendekezo hilo limefanywa wakati mawaziri hao wakikutana jijini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa mkutano wa AU, katika mkutano uliosimamiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Kamishna wa masuala ya amani na usalama katika AU, na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukanda wa Maziwa Makuu.

Washiriki katika mkutano huo wamepewa taarifa kuhusu matukio ya hivi karibuni ya kisiasa na kiusalama katika nchi za DRC, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Sudan Kusini, na wakakaribisha uchaguzi wa hivi karibuni Tanzania na ufanisi katika mchakato wa amani Sudan Kusini, na hatua zilizopigwa katika harakati za amani CAR.