Skip to main content

Jamii ya kimataifa ina wajibu wa kusaidia nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Syria- ILO

Jamii ya kimataifa ina wajibu wa kusaidia nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Syria- ILO

Wakati kongamano la wahisani wa Syria likiandaliwa kufanyika jijini London wiki ijayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, Guy Ryder, amesema ni wajibu wa msingi wa jamii ya kimataifa kuzisaidia nchi zinazowahifadhi wakimbizi wa Syria ili ziweze kukidhi changamoto za kiuchumi na kijamii zinazoletwa na mzozo wa wakimbizi hao.

Bwana Ryder amesema hayo mjini Amman, Jordan, ambako yupo ziarani kujionea moja kwa moja athari za mmiminiko wa idadi kubwa ya wakimbizi kwa soko la ajira, pamoja na kujadili fursa mbadala za ajira kwa wakimbizi na jamii zinazowapa hifadhi.

Bwana Ryder amesema ajira kwa wakimbizi na jamii zinazoubeba mzigo mkubwa wa kuwapa hifadhi, limeibuka kuwa suala nyeti katika juhudi za kimataifa za usaidizi kwa wakimbizi wa Syria, ambazo zimebadilika sasa kutoka usaidizi wa kibinadamu tu na kujumuisha mtazamo wa maendeleo.

Amesema changamoto ni kwa jamii ya kimataifa  kutoa usaidizi, rasilmali na ushauri kuhusu sera, ambao utawezesha serikali ya Jordan na nchi zingine kukidhi changamoto za jitihada za kuwasaidia wakimbizi, na wakati huo huo kuwawezesha wakimbizi wa Syria kujikimu kimaisha.