Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na wataalamu wa Afrika wamemtaka Rais wa Sierra Leone kusaini muswada wa utoaji mimba salama

UM na wataalamu wa Afrika wamemtaka Rais wa Sierra Leone kusaini muswada wa utoaji mimba salama

Kundi la tume za haki za binadamu za Umoja wa Mataifa na Afrika leo wamemtaka Rais wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma, kuokoa maisha ya mamilioni ya wanawake kwa kutia saini muswada wa utoaji mimba wa mwaka 2015 ili uanze kufanya kazi bila kuchelewa zaidi.

Wataalamu hao wameonya kwamba kusita kuondoa sheria ya utoaji mimba katika baadhi ya sehemu ikiwemo mashirika ya kidini, kumesababisha ucheleweshaji wa kutia saini muswada kwa Rais kuurejesha tena bungeni kwa ajili ya kufikiriwa upya.

Muswada wa 2015 wa utoaji mimba salama uliopitishwa na bunge la Sierra Leone mwezi desemba mwaka jana una lengo la kuhakikisha wanawake na vigori wanapata fursa ya huduma salama kuhusiana na utoaji mimba na kuidhinisha utoaji huo kwa sababu yoyote ile hadi muda wa wiki 12, na pia katika hali ya visa vya kubakwa, kuharibika kwa kijusi na pale ambapo afya ya mama iko hatarini aruhusiwe kutoa hadi ikiwa na wiki 24.

Wataalamu hao wameongeza kuwa muswada huu ni sheria ya msingi ili kuendeleza haki za afya kwa wanawake na vigori ikiwa ni pamoja na haki za ngono na uzazi katika nchi ambayo viwango vya vifo vya wajawazito ni miongoni mwa idadi ya juu zaidi duniani.