Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kunyonyesha kunapunguza vifo kwa watoto na saratani kwa kina mama: UNICEF

Kunyonyesha kunapunguza vifo kwa watoto na saratani kwa kina mama: UNICEF

Mfululizo wa nyaraka zilizochapishwa na jarida la kitabibu la The Lancet la Uingereza zinatoa ushahidi kwamba kuimarisha mazoea ya kunyonyesha kunaweza kuokoa maisha ya watoto zaidi ya 820,000 kwa mwaka, huku 9 kati 10 wakiwa ni watoto wachanga wa umri wa chini ya miezi sita. Hii ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Kuongeza unyonyeshaji kunaweza kuzuia karibu nusu ya visa vya kuhara na theluthi ya maradhi ya kupumua, magonjwa mawili ambayo yanaongoza kwa vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka 5.

Nyakara hizo za The Lancet pia zinaonyesha kwamba kila mwaka mama anayenyonyesha hatari yake ya kupata saratani ya matiti inapungua kwa asilimia 6. Kiwango cha sasa cha unyonyeshaji kimeshazuia takribani vifo 20,000 vya saratani ya matiti kila mwaka, idadi ambayo inaweza kuongezeka mara mbili kwa kuimarisha mazoea ya kunyonyesha.

Kwa mujibu wa mkuu wa lishe wa UNICEF Werner Schultink, uwekezaji katika unyinyeshaji una faida kubwa kwa wanawake na watoto na pia katika uchumi kwa nchi zote tajiri na masikini. Kwani imedhihirika kuwa unaboresha afya,ukuaji na maendeleo, na unachangia kuwa na mustakhbali endelevu.

Na hasara ya kutonyonyesha ni kubwa kwa nchi zote tajiri na masikini zikipoteza jumla ya dola bilioni 302 kila mwaka.

UNICEF inasema kunyonyesha ni nia bora ya asili, isiyo na gharama, inayojali mazingira na iliyo tayari wakati wote kwa kuwapa watoto wote masikini na tajiri afya njema mwanzo wa maisha yao jambo ambalo ni faida kwa pande zote.