Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naibu mkuu wa MONUSCO atembelea Ituri

Naibu mkuu wa MONUSCO atembelea Ituri

Naibu Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, MONUSCO, Mamadou Diallo ametimiza ziara ya siku mbili Kaskazini Mashariki mwa nchi kwenye jimbo la Ituri.

Taarifa iliyotolewa na OCHA inaeleza kwamba ametembelea maeneo ya Geti, Bukiringi na Komanda ambapo vitendo vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu vimeripotiwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, na kusababisha watu wapatao 200,000 kuhama makwao.

Bwana Diallo ambaye pia ni Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu ameelezea wasiwasi wake kuhusu mahitaji ya kibinadamu ya raia wa maeneo hayo, ambayo baadhi yao hayajatimizwa.

Amesisitiza kwamba jukumu la msingi la mamlaka za serikali ya DRC, vikosi vya usalama vya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo na mashirika ya kibinadamu ni kulinda raia, akiwasihi wahisani kutoa ufadhili ili kuwezesha wadau wote wa masuala ya kibinadamu kutimiza majukumu yao.