Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali Somalia

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limefanya kikao leo Alhamis kujadili hali nchini Somalia, ambapo Mwakilishi mpya wa Katibu Mkuu nchini humo, Michael Keating, amesema kuwa ingawa hali ya usalama bado inatoa changamoto kubwa, muafaka mpya wa kuleta nuru umefikiwa leo. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Akilihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Addis Ababa, Bwana Keating ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, ametangaza kuwa Baraza la Mawaziri la Somalia hatimaye hii leo limefikia muafaka kuhusu  mfumo wa kuendesha uchaguzi ujao baadaye mwaka huu.

Bwana Keating amesema uamuzi huo ambao haukuwa rahisi kufikiwa, ni hatua muhimu kwa Somalia na kwa serikali kuu ya taifa hilo.

(Sauti ya Keating)

“Mfumo huo unaweka bunge la chini la wabunge 275, ukilenga kuendeleza mtindo 4.5 wa kugawana mamlaka baina ya kaya, na bunge la juu la wanachama 54, kulingana na uwakilishi wa majimbo yaliyopo, yanayoibuka na yanayotarajiwa. Huu, Bwana rais ni mfumo uliobuniwa na Wasomali. Unaongozwa na Wasomali, na unamilikiwa na Wasomali.”

Hata hivyo, ameonya kuwa kutakuwa na vizuizi njiani, ambavyo wadau watatakiwa kukabiliana navyo ili waibuke na ushindi.