Mapigano Jebel Marra, Darfur yawalazimu maelfu kukimbia makwao

27 Januari 2016

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan, Marta Ruedas, ameeleza kutiwa wasiwasi na athari za mapigano katika eneo la Jebel Marra katika jimbo la Darfur nchini Sudan, ambako takriban watu 19,000 wamekimbilia jimbo la Darfur Kaskazini, huku wengine 15,000 wakikimbilia jimbo la Darfur ya Kati katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Eneo la Jebel Marra linapatikana katika majimbo matatu ya Darfur.

Bi Ruedas amesema, ingawa inatia moyo kuona kwamba usaidizi wa kibinadamu angalau unatolewa, juhudi zaidi zinahitajika, akitoa wito wahudumu wa kibinadamu wawezeshwe kuwafikia wahitaji salama na bila vikwazo.

Bidhaa muhimu za kuokoa maisha, mathalan nyongeza ya lishe kwa watoto, dawa na maji safi, zimetolewa kwa baadhi ya watu waliolazimika kuhama upya Darfur Kaskazini, na wadau wa kibinadamu wanatoa misaada kwa watu waliofurushwa makwao Darfur ya Kati.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter