Baraza la usalama halijajitahidi vya kutosha kuhusu Syria- OCHA

Baraza la usalama halijajitahidi vya kutosha kuhusu Syria- OCHA

Leo Baraza la Usalama limejadili hali ya kibinadamu nchini Syria, mzozo nchini humo ukikaribia kuingia mwaka wa sita na ripoti zikionyesha kwamba hali inazidi kuzorota.

Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Usalama, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA Stephen O’Brien amesema OCHA inakadiria kuwa watu wapatao milioni 4.5 hawafikiwi na misaada ya kibinadamu kwenye maeneo yaliyokumbwa na mapigano makali, miongoni mwao nusu milioni wakikumbwa na njaa kwenye maeneo yaliyozingirwa.

Bwana O’Brien amesisitiza kwamba pande kinzani katika mzozo zinadharau haki ya kimataifa ya kibinadamu inayolinda raia na mashirika ya kibinadamu, pande hizo zikishindwa kuhakikishia usalama wa misafara ya misaada.

Halikadhalika akanyooshea kidole  Baraza la Usalama akisema halijajitahidi vya kutosha akisema

(Sauti ya O’Brien)

“Lakini mauaji, mateso, uharibifu tele na dharau kwa sheria havipaswi  kuangaziwa kama mambo ya kawaida. Janga hili limetengenezwa na binadamu. Linatisha lakini linaweza kuzuiliwa. Na sisi – nyie – mnapaswa kushikamana kupambana nalo.”  

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP, Ertharin Cousin amesisitiza tatizo la ufikishaji misaada kwenye maeneo yaliyozingirwa akisema msafara uliofika Madaya wiki iliyopita hautatosha kuzuia janga la njaa nchini humo.

Amesema mashirika ya kibinadamu yanapaswa kuruhisiwa kusafiri kwa usalama,uwazi na bila kibali kwenye maeneo yote yanayohitaji usaidizi.