Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila uwekezaji uwe jawabu kwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi- Ban

Kila uwekezaji uwe jawabu kwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi- Ban

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika mkutano wa viongozi wa uwekezaji katika sekta binafsi lengo likiwa ni kuangalia hatari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya biashara.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema amesimama mbele ya wawekezaji hao akiwa na matumaini mapya kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma unaweza kukabili changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema katika zama za sasa za changamoto, wawekezaji hao wana rasilimali pekee ya kukabilia na kuhimili mabadiliko hayo, akiitaja rasilimali hiyo kuwa ni uongozi wao thabiti.

Ban amesema uongozi wa wawekezaji katika kuelekeza rasilimali katika vitegauchumi vinavyotoa kiwango kidogo cha hewa ya ukaa, ni hatua pekee katika karne hii ya 21.

Amesema kila dola lazima iwekezwe kwenye kuzalisha huduma na bidhaa zinazotoa kiwango kidogo cha hewa ya ukaa.

Ameongeza kuwa sekta binafsi ni injini ambayo itachochea majawabu yanayohitajika kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi, kumaliza umaskini wa nishati na kuweka mustakhbali salama zaidi kwa kizazi cha sasa na vijavyo.