Ahadi za serikali mpya ya Tanzania kubana matumizi zaridhisha IMF

Ahadi za serikali mpya ya Tanzania kubana matumizi zaridhisha IMF

Matarajio ya kiuchumi ya Tanzania yanatia matumaini sana, amesema leo mkuu wa Ujumbe wa Shirika la Fedha Duniani, IMF, Hervé Joly, huku serikali ya awamu ya tano ikiwa imeahidi kulipa malimbikizo kwa wanaotoa huduma.

Bwana Joly amehojiwa na idhaa hii wakati IMF imekamilisha tathmini ya tatu ya uchumi wa Tanzania kupitia mfumo wa PSI,ambao mapendekezo yake yanategemewa na wahisani.

Amesema hali ya kiuchumi nchini Tanzania ni nzuri, uchumi ukiwa umekuwa kwa asilimia 7 mwaka 2015 na ongezekeo la bei za bidhaa likiwa ni asilimia 5.6 tu.

Licha ya hayo, amesema IMF imekuwa na wasiwasi kuhusu bajeti ya serikali lakini amesema harakati zilizochukuliwa na serikali mpya zimetia matumaini.

(Sauti ya bwana Joly)

“Serikali mpya imetuma ujumbe mzuri ikiahidi kuleta mabadiliko kwenye serikali, kupunguza matumizi na kupambana na ukwepaji ushuru, Kuhusu bajeti na changamoto zake, wameonyesha nia yao ya kuirekebisha na tunadhani ni hatua nzuri kwa sababu itasaidia kupunguza madeni baadaye. Pia wataongeza vikwazo ili kuhakikisha wafanyakazi wa serikali hawaanzi kufanya matumizi kama pesa hazipo, na kwamba sheria hii inafuatiliwa.”          

Amesema matarajio ya ukuaji wa uchumi ni mazuri kwa mwaka 2016, IMF ikipendekeza kuendelea kuleta mabadiliko katika matumizi ya serikali na hasa kupunguza madeni ya TANESCO.