Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEP imetaka hatua zichukuliwe kulinda mali asili ya Afrika:

UNEP imetaka hatua zichukuliwe kulinda mali asili ya Afrika:

Naibu Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa mazingira UNEP Ibrahim Thiaw, ametoa wito wa ulinzi mzuri dhidi ya wanyamapori na mali asili tele ya Afrika kama njia ya kufanikisha ajenda ya Muungano wa Afrika AU ya mwaka 2063.

Akizungumza katika kikao cha faragha cha baraza la Muungano wa Afrika mjini Mekelle, Ethiopia, Bw. Thiaw amewaambia mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika kwamba thamani ya biashara haramu ya wanyamapori na mbao katika bara hilo ni karibu sawa na msaada rasmi wa maendeleo wa kimataifa kwa Afrika ODA.

Ameongeza kuwa maliasili nyingi ya Afrika inapotelea kwenye mikono ya mitandao ya wahalifu ambao wamejipenyeza barani humo, akisistiza kwamba maliasili hiyo ndio mustakhbali wa mataifa ya Afrika na kuziiba ni kuyanyima mataifa hayo uwezo wa kuchagua na kuamua mustakhbali wao na maendeleo ya kiuchumi kwa watu wao kama sehemu ya dunia.

Amewataka mawaziri hao wa Afrika kuanza kuchukua hatua kushughulikia suala hilo hususan kwa kujumisha utunzaji wa maliasili katika mtaala wa Afrika.