Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitendo vya ukiukaji wa haki vyaongezeka DRC

Vitendo vya ukiukaji wa haki vyaongezeka DRC

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imeorodhesha visa 347 vya ukiukaji wa haki za binadamu mwezi Disemba mwaka 2015 nchini humo.

Kwa ujumla, idadi ya visa hivyo imefika 3,877 mwaka uliopita, ikiwa ni ongezeko la asilimia 64 ikilinganishwa na mwaka 2014.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo, nusu ya vitendo hivyo vimetekelezwa na vikosi vya usalama vya serikali, huku zaidi ya askari 300 wa serikali wakiwa wameshtakiwa kwa vitendo hivyo mwaka 2015.

Hata hivyo ofisi ya haki za binadamu imeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu vitendo vya ukiukaji wa haki vinavyohusiana na mchakato wa uchaguzi, ikisema hakuna askari yeyote aliyeshtakiwa kutokana na uhalifu huo hadi sasa, huku visa vikiwa vimeripotiwa zaidi kwenye majimbo ambapo vyama vya upinzani vina ushawishi mkubwa zaidi.