Skip to main content

UM na mashirika ya misaada waomba dola milioni 298 kwa ajili ya wakimbizi Iraq:

UM na mashirika ya misaada waomba dola milioni 298 kwa ajili ya wakimbizi Iraq:

Kukiwa hakuna mwangaza wa kuitisha vita nchini Syria Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu na mae ndeleo nchini Iraq wametoa ombi la dola milioni 298 kwa ajili ya kuendelea na msaada kwa takribani wakimbizi 250,000 wa Syria walioko nchini Iraq.

Ombi hilo limetolewa katika uzinduzi wa mpango wa ukurasa mpya wa Iraq katika kusaidia wakimbizi wa Syria kikanda ujulikanao kama 3RP uliofanyika mjini Erbili. Watu mbalimbali wamehudhuria uzinduzi huo akiwemo Dr. Ali Sindi, waziri wa mipango wa serikali ya kikanda ya Kurdistan.

Pia wengine waliohudhuria ni pamoja na mawaziri, maafisa wa serikali, mashirika ya misaada ya kibinadamu na wahisani wanaosaidia wakimbizi wa Iraq. Jimbo la Kurdistan linahifadhi asilimia 97 ya wakimbizi wa Syria pamoja na wakimbizi wa ndani Zaidi ya milioni moja waliosambaratishwa na vita nchini Iraq.

Msaada huo unaohitajika ni kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma ya mahitaji ya lazima kwa wakimbizi hao, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na kuzisaidia jamii zinazowahifadhi wakimbizi.

Pia itasaidia katika masuala ya elimu na kuongeza mafunzo ya vitendo ili kuboresha maisha ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.