Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na wadau wa kibinadamu waomba pande kinzani Syria ziwezeshe kuwafikia wahitaji

UM na wadau wa kibinadamu waomba pande kinzani Syria ziwezeshe kuwafikia wahitaji

Viongozi wa Mashirika ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, wametoa wito kwa pande kinzani nchini Syria zikomeshe mapigano na kuruhusu wahudumu wa kibinadamu kuwafikia watu wanaohitaji usaidizi wa kibinadamu.

Miongoni mwa waliotoa wito huo ni Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu nchini Syria, Yacoub El Hillo, ambaye amesema mateso wanayopitia watu wa Syria ni makubwa mno, akiongeza kwamba …

“Tunatoa ujumbe dhahiri kwa wanaokuja Geneva, kwamba na itoshe! Wasyria hawawezi tena kuendelea kuibeba gharama ya kufeli kisiasa. Asilimia 67 ya watu wa Syria wanaishi katika umaskini sasa, huduma zikivurugwa kila siku, shule zikishambuliwa kila siku, na chanjo haitolewi ipasavyo.”

Naye Mkurugenzi wa Operesheni katika Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, John Ging, amesema ana matumaini sasa kufuatia kutangazwa hapo jana kuwa wawakilishi wa pande kinzani za Syria watakutana jijini Geneva, Uswisi mwishoni mwa wiki hii, na kwamba mchakato huo wa kisiasa utaleta suluhu litakaloumaliza mzozo wa kibinadamu nchini Syria.