Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukuaji wa uchumi pekee si hakikisho la uwepo wa ajira zenye utu: ILO

Ukuaji wa uchumi pekee si hakikisho la uwepo wa ajira zenye utu: ILO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kazi duniani, ILO Guy Ryder amesema misukosuko ya uchumi katika nchi za kundi la BRICS inaweza kufuta mafanikio yaliyokwishapatikana katika kuwezesha uwepo wa kundi la watu wa kipato cha kati.

Amesema hayo mjini Ufa huko Urusi katika mkutano wa kwanza mawaziri wa kazi wa nchi zinazounda kundi hilo ambazo ni Brazil, Urusi, India, Uchina, na Afrika Kusini.

Bwana Ryder pamoja na kutambua mafanikio ya hivi karibuni ya nchi za BRICS kuwa kichochea cha ukuaji duniani wa watu wa daraja la kati, amesema kutokana na mwelekeo wa sasa wa uchumi duniani, kundi hilo linaweza kujikuta katika umaskini iwapo hatua sahihi hazitachukuliwa.

Amesema ni vyema kutambua kuwa ukuaji wa uchumi pekee kwa nchi siyo suluhu bali kuweka mazingira ya kuhakikisha ukuaji huo unawezesha upatikanaji wa ajira zenye utu, uwiano wa ajira na hata ujumuishaji wa makundi yote kwenye jamii.

Kwa mantiki hiyo amesisitza uwekezaji thabiti wa umma kwenye miundombinu ili kukuza fursa za ajira bila kusahau kuhakikisha kuna uhusiano kati ya taasisi zinazotoa elimu na waajiri ili elimu ikidhi mahitaji ya soko.