Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 550 zahitajika kusaidia wahamiaji na wakimbizi Ulaya:UNHCR&IOM

Dola milioni 550 zahitajika kusaidia wahamiaji na wakimbizi Ulaya:UNHCR&IOM

Wakati vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati na kwingineko vikizidi kuwafungisha virago watu na kuelekea Ulaya kuomba hifadhi , Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR) na lile la Kimataifa la Uhamiaji(IOM) na washirika wao 65 wametoa ombi la dola milioni 550 ili kusaidia mahitaji ya kibinadamu ya watu hao wanaoingia Ulaya.

Kwa mujibu wa mashirika hayo mwaka 2015 umeshuhudia zaidi ya wakimbizi na wahamiaji milioni moja wakiwasili Ulaya kwa njia ya boti, huku zaidi ya laki nane na nusu wakitoka Uturuki na kuingia Ugiriki na wengine wakiendelea na safari kuelekea Austria, Ujerumani, Sweden na nchi zingine.

Lengo la ombi hilo ni kufadhili operesheni za kibinadamu kwa mwaka 2016 kwa nchi zilizoathirika na kupokea wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji huku nusu ya fedha zitapewa Ugiriki.