Skip to main content

Mapigano huko Darfur yashuhudiwa zaidi wakati huu: Ladsous

Mapigano huko Darfur yashuhudiwa zaidi wakati huu: Ladsous

Leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili hali ya usalama, kisiasa na kibinadamu kwenye eneo la Darfur nchini Sudan, huku mashambulizi dhidi ya raia na mapigano baina ya serikali na vikundi vilivyojihami yakiwa yameongezeka tena mwezi huu. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mbele ya Baraza la Usalama, mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja huo Hervé Ladsous ameeleza kwamba Ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa Darfur, UNAMID umeshuhudia mapigano mashariki, kaskazini na katikati ya Darfur, askari wa UNAMID wakiwa wameshambuliwa mara mbili mwezi huu tu. Aidha amesema UNAMID na mashirika ya kibinadamu yanategemea kwamba idadi ya wakimbizi wa ndani itaongezeka zaidi.

Hata hivyo amesema UNAMID haikuweza kuthibitisha idadi ya wahanga, serikali ya Sudan ikiendelea kuzuia UNAMID katika operesheni zake, hadi kunyima viza kwa wafanyakazi wake.

Ameongeza kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kutayarisha mkakati wa kuondoa UNAMID Darfur iwapo mwelekeo utakuwa mzuri akisema

(Sauti ya Bwana Ladsous)

“ Tunategemea kwamba serikali ya Sudan itajitahidi kupiga hatua zitakazopimika katika maswala muhimu zikiwemo usitishwaji mapigano, mchakato jumuishi wa amani, usafiri huru wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kibinadamu. Hizo ni hatua za msingi kabla ya kuanza mazungumzo zaidi kuhusu kupunguza askari wa UNAMID.”