Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu yazidi kuzorota Yemen: McGoldrick

Hali ya kibinadamu yazidi kuzorota Yemen: McGoldrick

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Yemen, Jamie McGoldrick amesema juhudi za kuzifikia wilaya tatu zinazohitaji misaada ya kibinadamu nchini humo zinaendelea, ambapo mazungumzo na pande kinzani yanasongeshwa.

Katika taarifa yake kuhusu ziara ya hivi karibuni nchini humo, kiongozi huyo amesema alijionea hali halisi ya kibinadamu na sasa wanasaka namna ya kuyafikia maeneo kusudiwa kwa kusihi pande husika kuruhusu bila masharti.

Akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa kuhusu msafara wa misaada iliyofika kwenye eneo hilo akasema..

(Sauti ya Jamie)

“ Tunatumai kwamba mafanikio haya ya mara moja yatakuwa siyo ya mara moja tu, na tunatumai kwamba tunaweza kuendelea kwa njia ya kawaida kwa sababu ni njia ya pekee tutaweza kusaidia raia, pia tunapaswa kuwezesha sekta binafsi kufufuka ndani ya maeneo hayo yaliyozingirwa.”

Bwana McGoldrick amesema katika wilaya hizo tatu, ameshuhudia madhara ya machafuko kwa raia hususani katika miundombinu, na maisha ya kijamii kwa ujumla mathalani ametaja kuwa maduka machache yamefunguliwa hali inayofanya wananchi kuwa katika hali mbaya nchini Yemen.

Amesisitiza kuwa mahitaji ya msingi kama vile chakula hayapatikani, huku pia mafuta kwa ajili ya usafiri na maji vikiwa adimu. Huduma za afya nazo zimekumbwa na mkwamo kwani hospitali kam vile Al Thawra imeshambuliwa mara kadhaa na hivyo kukumbwa na upungufu wa madawa.

Mkuu huyo wa masuala ya kibinadamu nchini Yemen, ametaka maeneo nyeti kama hospitali na huduma nyingine za kijamii yalindwe kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.