Kaskazini mwa Mali kwahitaji uwekezaji zaidi

Kaskazini mwa Mali kwahitaji uwekezaji zaidi

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Sahel, Toby Lanzer amemaliza leo ziara yake nchini Mali ambapo ametembelea maeneo ya kaskazini mwa nchi yaliyokumbwa na mzozo wa kisiasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, Bwana Lanzer ametambua mafanikio yaliyopatikana katika kujeresha huduma za elimu, maji na afya na kumulika changamoto zilizobaki, ikiwemo kueneza utawala wa mamlaka za serikali.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Maifa baada ya ziara hiyo, Bwana Lanzer  amesisitiza majukumu ya serikali ya Mali.

(Sauti ya Bwana Lanzer)

"Nadhani ni vizuri na muhimu sana kwa ajili ya utulivu na maendeleo  kuwa serikali itawekeza kwa usawa na uwiano zaidi, kwa raia wote wawe Mashariki, Magharibi, Kaskazini au Kusini."

Aidha OCHA imeeleza kwamba mashirika ya kibinadamu yamefikisha misaada kwa zaidi ya watu milioni moja na nusu mwaka iliopita, huku ikieleza kwamba kwa ujumla yanahitaji dola milioni 345 mwaka huu.