Hali ya usalama Burundi tofauti na tunavyosikia- Balozi Martin

Hali ya usalama Burundi tofauti na tunavyosikia- Balozi Martin

Wanachama wa Baraza la Usalama wamekutana leo na rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na wamejadili hali ya usalama nchini humo pamoja na mchakato wa mazungumzo ya amani yanayoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuongozwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Hiyo ni kwa mujibu wa Balozi Ismael Martins mwakilishi wa kudumu wa Angola kwenye Umoja wa Mataifa ambaye naye ni miongoni mwa wajumbe wa Baraza walioko ziarani nchini humo.

Akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya simu Balozi Martins amesema pamoja na mazungumzo na Rais Nkurunzinza yaliyofanyika mkoa wa kati wa Gitega, wakiwa njiani wanasafiri hawakuweza kuthibitisha madai yote ya ukosefu wa usalama akisema

(Sauti ya Balozi Martins)

« Wacha niseme kwamba niko hapa, tumerudi kutoka mkutano huo na rais, tayari ni saa mbili za usiku, tunasafiri kwa njia ya barabara na hatujaona hali ambayo mara nyingi inahadithiwa kwamba hali ya usalama imezorota nchini kote.»

Amesema kutoka Burundi wanaelekea Ethiopia ili kujadili na Muungano wa Afrika kuhusu hali ya Somalia na utaratibu wa mazungumzo ya amani nchini Burundi.

Kuhusu nia ya Muungano wa Afrika ya kutuma ujumbe wa ulinzi wa amani nchini Burundi, na msimamo wa Burundi wa kukataa ujumbe huo, Balozi Martins amesema mazungumzo yataendelea na Rais wa Burundi ili kupata mwafaka na kurejesha utulivu nchini humo hata kama ujumbe hautatumwa Burundi.