Skip to main content

Hali ya usalama Kivu Kaskazini yatia wasiwasi

Hali ya usalama Kivu Kaskazini yatia wasiwasi

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa usaidizi wa kibinadamu OCHA huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC imesema hali ya usalama kwenye jimbola Kivu Kaskazini inazidi kudorora na kutia wasi wasi mkubwa.

Rein Paulsen amesema kwa miezi kadhaa sasa hali inazidi kuwa mbaya huko Beni, Lubero, Masisi, Rutshuru na Walikale ambako kuna ripoti za kutekwa kwa watoa misaada, raia na kwamba mashambulizi dhidi ya misafara yenye mahitaji muhimu yameongezeka.

Amesema hayo hiyo imesababisha usitishaji wa mgao wa misaada akitolea mfano kuwa tarehe 20 mwezi huu shirika lisilo la kiserikali la madaktari wasio na mipaka, MSF lililazimika kufunga mradi wake wa matibabu huko Mweso, eneo la Masisi baada ya misafara ya magari yake yenye shehena za misaada kuporwa na wafanyakazi wake kutekwa mwezi Disemba.

Bwana Paulsen amesema bila ya hatua za dharura za ulinzi wa watoa misaada ya kibinadamu, OCHA na wadau wake watashindwa kulinda raia ambao ndio jukumu lao.

Wametoa wito kwa serikali ya DRC na wadau wengine husika kuchukua hatua kuimarisha usalama ili operesheni za usaidizi ziendele.

Zaidi ya watu Milioni 7.5 nchini DRC wanahitaji misaada ya kibinadamu.