Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ya kudumu Nigeria ihusishe ujumuishaji wanawake na watoto kwenye jamii

Amani ya kudumu Nigeria ihusishe ujumuishaji wanawake na watoto kwenye jamii

Wataalamu watatu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa serikali ya Nigeria kuhakikisha mipango ya kuboresha jamii hasa zile zilizokumbwa na mashambulizi ya Boko Haram, zinahusisha kujumuisha wanawake na watoto.

Katika taarifa yao ya pamoja baada ya kuhitimisha ziara yao nchini Nigeria, wataalamu hao wamesema hatua hiyo itahakikisha uboreshaji huo unawezesha kupatikana kwa amani ya kudumu.

Miongoni mwao Urmila Bhoola ambaye anahusika na haki ya afya amesema wakati ukanda huo ukiwa kwenye mpito wa kutoka kwenye usaidizi kwenda kujikwamua ni muhimu kuhakikisha mikakati inazingatia haki za binadamu na athari za mzozo huo kwa wanawake na watoto.

Amesema pamoja na kutaka kuboresha jamii ni lazima hatua zizingatie mahitaji ya wakati huu ya wanawake na watoto wa kike.

Pamoja na kupongeza hatua za serikali ya Nigeria za kuimarisha jamii zilizoathiriwa na mashambulizi ya Boko Haram, watalaamu hao wamesema bado kuna pengo katika utekelezaji na usimamizi wa sera na sheria za kujumuisha wanawake na watoto kwenye jamii, mathalani upatiaji huduma wanawake wahanga wa mashambulizi ya Boko Haram.

Wakati wa ziara hiyo wataalamu hao walikutana na wawakilishi wa serikali na vikundi vya kiraia pamoja na familia za wasichana wa Chibok waliotekwa na Boko Haram.

Ripoti yao ya ziara hiyo ya siku Tano itawasilishwa mbele ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa baadaye mwaka huu.