Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Zimbabwe kwa kuharamisha ndoa za utotoni

Heko Zimbabwe kwa kuharamisha ndoa za utotoni

Umoja wa Mataifa nchini Zimbabwe umekaribisha  uamuzi wa mahakama ya kikatiba nchini humo wa kuharamisha ndoa kwa watoto ambao ni watu wenye umri wa chini ya miaka 18.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF mjini Harare imesema uamuzi huo wa kihistoria utasaidia kusongesha haki za mtoto na hivyo kumaliza utamaduni huo wa kuoza watoto mapema hususan watoto wa kike.

Halikadhalika imesema uamuzi huo wa mahakama sio tu unaendeleza katiba bali pia unasisitiza azma ya Zimbabwe ya kusimamia mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto na chata ya Afrika kuhusu haki na ustawi wa mtoto.

Tafiti nchini Zimbabwe zinaonyesha kuwa asilimia karibu 33 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 20 na 49 waliozwa wakiwa na chini ya umri wa  miaka 18 na hivyo siyo tu kuhatarisha utu wao bali pia ustawi wao hasa kupata elimu.

Umoja wa Mataifa umesema uamuzi wa sasa unachochea umuhimu wa kurekebisha sheria ya ndoa nchini Zimbabwe na ile ya ndoa za jadi ili ziende sambamba na katiba ya nchi.